
Nukta: Namna Umeme Vijijini Unavyoweza Kutumika Kuchochea Maendeleo
Imeandaliwa na Daniel Mwingira
Arusha. Wakati wanawekewa umeme kwa mara ya kwanza, wananchi wengi wa vijijini huamini ujio wa nishati hiyo huja na fursa lukuki zinazopatikana kirahisi lakini siyo wote hufanikiwa kutimiza fikra hizo.
Ukiachana na matumaini ya wananchi, Mtaalamu wa dhana ya umeme kwa matumizi ya uzalishaji mali kutoka Energy Change Lab, Fredrick Mushi anaeleza kuwa hapo awali hata sehemu kubwa ya wawekezaji nao walifikiri hivyo pia.
“Wawekezaji binafsi au REA (Wakala wa Nishati Vijijini) walifikiri wanapopeleka umeme vijijini basi shughuli za uchumi zingejitokeza zenyewe kama ilivyo mjini.
Wengi waliofikiwa na umeme vijijini bado wanatumia zaidi kuwasha taa na kuchaji simu badala ya kufanya shughuli za uzalishaji.
Lakini imeonekana sehemu kubwa ya matumizi ya umeme ni ya mwanga, kuchaji simu, kuwasha radio au Television,” anasema Mushi kando ya tamasha la Energy Safari 2018 lililofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Pamoja na matumaini makubwa juu ya fursa za kiuchumi zinazojitokeza kutokana na upatikanaji wa umeme, wajasiriamali wengi wa vijijini hukumbana na changamoto katika kuchangamkia fursa hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uelewa hafifu wa namna ya kutumia nishati hiyo na kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya mwaka 2016 iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaeleza kuwa mwaka huo theluthi moja (asilimia 32.8) ya kaya zote nchini ilikuwa ikipata huduma ya umeme. Kati ya kaya hizo zinazopata umeme, tatu kwa kila nne (asilimia 74.9) zimeunganishwa na umeme kutoka katika gridi ya Taifa, takribani robo (asilimia 24.7) zinapata kutoka katika umemejua na asilimia 0.3 tu zinapata umeme kutoka vyanzo vingine vya nishati hiyo.
Bofya hapa kusoma zaidi, nakala hii imetayarishwa na Daniel Mwingira | http://nukta.co.tz